Kiongozi wa chama kipya cha upinzani nchini Korea Kusini azuru Visiwa vya Takeshima vinavyozozaniwa

Kiongozi wa chama cha upinzani cha pili kwa ukubwa nchini Korea Kusini amezuru Visiwa vya Takeshima katika Bahari ya Japani.

Korea Kusini inavidhibiti. Japani inadai kuvimiliki na inasema Korea Kusini inavitwaa kinyume cha sheria.

Chama kipya cha Rebuilding Korea kilishinda viti 12 kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu. Kinaongozwa na Waziri wa zamani wa Sheria Cho Kuk, aliyewasili katika kile ambacho Korea Kusini inakiita Visiwa vya Dokdo jana Jumatatu.

Cho alitoa taarifa akidai visiwa hivyo ni eneo la Korea Kusini.

Pia alimkosoa Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol kwa sera zake kuelekea Japani.

Mwezi Aprili mwaka huu, baadhi ya wanachama wa chama kikuu cha
upinzani cha Democratic pia walizuru visiwa hivyo. Chama hicho,
kilichoshinda viti vingi katika uchaguzi wa mwezi Aprili, kilipinga sera za Yoon kuhusu Japani.