Kushika nafasi kwa kulipa ada kwaleta tumaini la kumaliza foleni migahawani

Kampuni moja nchini Japani imeendeleza mfumo wa kushika nafasi kwa kulipa ada kwa ajili ya migahawa. Watumiaji wengi wanaotumia mfumo huo ni watalii wa kigeni wenye shughuli nyingi ambao hawataki kusubiri kwenye foleni.

Kampuni ya IT yenye makao yake jijini Tokyo ilianzisha kile inachokiita “FastPass” mwezi Februari mwaka huu. Mfumo huo unatoa tumaini la kumaliza tatizo la muda mrefu wa kusubiri migahawani.

Nusu ya viti kwenye mgahawa wa rameni jijini Tokyo vimeunganishwa na mfumo huo. Mgahawa huo unasema takribani asilimia 50 ya watumiaji ni wasafiri wa kigeni.

Wanashika nafasi zao mtandaoni. Ada ni yeni 390, au takribani dola 2.50 kwa kila mtu.

Mtalii kutoka Canada anasema, “Ni kama dola 3 au 4 (za Canada) kwa kila mtu. Kwa hivyo, sioni shida kama itasaidia kuharakisha mchakato wa kula haraka.”

Taniguchi Yu ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya TableCheck inayotoa huduma hiyo. Anasema: “Muda ni kitu cha thamani kwa watalii. Wengi wao wanaona wanaweza kuwa wakifanya kitu kingine kuliko kusubiri kwenye foleni mgahawani. Tunapata mrejesho mzuri.”

Migahawa zaidi ya kumi imejiunga na huduma hiyo. Kampuni inayotoa huduma hiyo inalenga kuongeza idadi hiyo hadi karibu 300 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.