Mauzo ya magari ya China yapanda kutokana na umaarufu wa aina za gari zinazotumia 'nishati mpya'

Mauzo ya magari mapya ya China yaliongezeka mwezi Aprili kutoka mwaka mmoja uliopita kutokana na mauzo ya haraka ya magari yanayotumia mfumo wa umeme au EV na mengine yanayoitwa "magari yanayotumia nishati mpya."

Chama cha Watengenezaji Magari cha China kinasema magari milioni 2.35 yalitolewa kutoka kwenye karakana za wafanyabiashara mwezi uliopita. Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 9.3.

Kuhusu mauzo ya nje, China ilisafirisha magari 504,000 mwezi Aprili. Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 34 kutoka mwaka jana.

Kasi hiyo inazidi kwa kiasi kikubwa ile ya mwaka jana wakati China ilipokuwa muuzaji mkubwa zaidi wa magari duniani.

Lakini maafisa katika nchi za Magharibi wanashuku kuwa magari ya Wachina yanauzwa kwa bei ya chini isivyo kawaida katika masoko ya ng'ambo kutokana na uzalishaji kupita kiasi, miongoni mwa sababu nyinginezo.