Zelenskyy: Mashambulizi ya Urusi dhidi ya Kharkiv yanalenga kudhoofisha vikosi vya Ukraine

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema mashambulizi ya Urusi ya kuvuka mpaka kwenye eneo la Kharkiv mashariki mwa nchi hiyo yanalenga kudhoofisha vikosi vya Ukraine huku mapigano makali yakiendelea katika eneo la Donetsk.

Zelenskyy alisema hayo katika video iliyotolewa jana Jumapili.
Alisema operesheni za mapigano makali zinaendelea katika maeneo mengi huko Donetsk pamoja na vita huko Kharkiv. Alikiri hali ngumu wanayopitia Ukraine lakini akasema itaweza kuzuia mashambulizi ya Urusi.

Vikosi vya Urusi vilivyovuka mpaka kutoka kaskazini vinaongeza operesheni za mashambulizi huko Kharkiv. Jana Jumapili wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema ilitwaa maeneo mengine manne.

Gavana wa eneo la Kharkiv alisema siku hiyo hiyo kwamba mashambulizi ya Urusi yalikuwa yakiendelea usiku na mchana kaskazini mwa eneo hilo.

Gavana huyo alisema raia wawili waliuawa, na katika muda wa siku mbili zilizopita takribani wakazi 4,000 walihama makazi yao.