Vikosi vya Israel vyafanya mashambulizi ya ardhini huko Jabalia huku idadi ya waliouawa ikifikia 35,000

Vikosi vya jeshi la Israel vimefanya mashambulizi ya ardhini kwenye mji wa Jabalia uliopo kaskazini mwa Gaza, huku vikiendelea na mashambulizi katika mji wa kusini wa Rafah. Jeshi la Israel linasema kundi la Kiislamu la Hamas linajaribu kujipanga upya mjini Jabalia.

Jana Jumapili, jeshi la Israel lilisema kwamba wanajeshi wake wa ardhini waliwaua wapiganaji 10 wa Hamas wakati wa mashambulizi huko Rafah.

Zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi yao wamejihifadhi kwa muda huko Rafah.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takribani watu 300,000 wamehama makazi yao kutoka Rafah. Umoja wa Mataifa unatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, ukisema kwamba hakuna sehemu salama katika Ukanda wa Gaza.

Jana Jumapili mamlaka za afya huko Gaza zilisema kwamba idadi ya vifo katika ukanda huo imefikia 35,034 tangu mzozo kati ya Israel na Hamas kuanza.