Aliyepandikizwa figo ya nguruwe afariki Marekani baada ya upandikizaji mwezi Machi

Madaktari bingwa wa upasuaji nchini Marekani wamesema aliyekuwa mgonjwa wa kwanza kupandikizwa figo ya nguruwe iliyoboreshwa jeni amefariki miezi miwili baada ya upasuaji wa kupandikizwa.

Hospitali Kuu ya Massachusetts imetoa tangazo hilo juzi Jumamosi. Haikutoa taarifa za kina, lakini imesema hakuna kiashiria kwamba kifo cha mgonjwa huyo kimetokana na upandikizwaji wa hivi karibuni.

Machi 16, timu ya madaktari wa upasuaji katika hospitali ya Boston ilimpandikiza ogani hiyo mwanaume mwenye shida ya figo. Alikuwa na umri wa miaka 62 wakati huo. Ogani hiyo iliboreshwa jeni ili kuepusha changamoto za mwili kukataa ogani hiyo mpya.

Mgonjwa huyo alipona vizuri na kuruhusiwa kwenda nyumbani mwezi Aprili.

Juhudi zinaendelea nchini Marekani za kuvumbua njia za kupandikiza ogani za nguruwe zilizoboreshwa jeni kwa binadamu.