Kundi la Haki za Kibinadamu: Utawala wa kijeshi wa Myanmar umeua watu 5,000 tangu 2021

Kundi la kutetea haki za kibinadamu nchini Myanmar linasema kuwa watu 5,000 wameuawa katika mashambulizi na ukandamizaji wa jeshi la nchi hiyo tangu lilipochukua mamlaka katika mapinduzi miaka mitatu iliyopita.

Chama cha Msaada kwa Wafungwa wa Kisiasa, ambacho pia kinajulikana kama AAPP, kimetoa takwimu yake ya idadi ya vifo, ikiwa ni pamoja na wanaharakati wanaounga mkono demokrasia na raia, hadi kufikia Ijumaa iliyopita.

Chama hicho kinasema watu wengi waliuawa katika eneo la kaskazini magharibi la Sagaing ambako mapigano yanaendelea kati ya wanajeshi na vikosi vinavyounga mkono demokrasia, na mji wa pili kwa ukubwa wa Mandalay.

Jeshi limedhibiti nchi hiyo tangu mapinduzi ya Februari 1, 2021, na kuendelea kuwaweka kizuizini wanachama wa vikosi vinavyounga mkono demokrasia.

Tangu msimu wa pukutizi mwaka jana, jeshi hilo limekuwa likipoteza mapambano kutokana na mashambulizi ya makundi yenye silaha ya makabila madogo kwa ushirikiano na vikosi vinavyounga mkono demokrasia karibu na mpaka. Wanajeshi wanazidisha mashambulizi ya anga.