Rangi za kupendeza zaonekana kote Hokkaido huko kaskazini mwa Japani

Rangi za kupendeza ama ‘Northern Lights’ zimeonekana kwenye mkoa wa kaskazini kabisa mwa Japani wa Hokkaido kuanzia jana Jumamosi usiku hadi mapema leo Jumapili asubuhi, kufuatia mfululizo wa milipuko ya miako ya jua pamoja na utoaji mkubwa wa korona.

Rangi hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘aurora borealis’ ziliipamba anga kwenye mji wa Nayoro uliopo kaskazini mwa Hokkaido. Anga ilianza kubadilika na kuwa na rangi ya zambarau majira ya saa moja usiku jana Jumamosi. Watu wengi walituma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii wakisema kuwa wameziona.

Kwenye Mji wa Rikubetsu huko mashariki mwa Hokkaido, kamera ya video ilichukua picha za anga la usiku likiwa limefunikwa na rangi za zambarau kuanzia machweo hadi alfajiri.

Afisa kwenye kituo cha uchunguzi katika mji zilipochukuliwa picha za video alisema mwanga huo unaaminika kuwa aurora ya latitudo ya chini huku anga nyuma ya mawingu iling’aa vizuri.

Mwongozaji wa kituo cha uchunguzi alibainisha kwamba miako ya Jua ilisababisha dhoruba za sumaku ya kijiografia, zinazoruhusu mwanga wa rangi kuweka onyesho la nadra katika eneo la latitudo ya chini kama Hokkaido.