Waandamanaji jijini Tel Aviv watoa wito kwa serikali kuhakikisha mateka wanaachiliwa

Maelfu ya watu wamekusanyika kwenye maandamano katika mji wa Tel Aviv nchini Israel jana Jumamosi. Wametoa wito kwa serikali kuangazia katika kuhakikisha mateka wanaachiliwa, badala ya kupanua oparesheni za kijeshi huko Gaza.

Washiriki wa maandamano hayo wanadai kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kujiuzulu ili kuwajibika kwa kushindwa kutatua suala la mateka.

Majadiliano yanayolenga kufikiwa kusitishwa kwa mapigano na kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka yamesitishwa, kutokana na Israel na Hamas kushindwa kukaa kwenye meza ya mazungumzo.

Vyombo vya habari vya Israel vimewanukuu maafisa wa Israel wakisema kwamba majadiliano yataendelea, kwani hayajashindikana kabisa.

Hamas ilisema kwenye taarifa yake kwamba itaangazia upya mikakati yake kwa ajili ya majadiliano.

Wakati huo huo, vikosi vya Israel vimekuwa vikiongeza shinikizo kwa Hamas kwa kupanua oparesheni zake za kijeshi mjini Rafah, huko kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Kwenye ujumbe mpya uliotolewa na jeshi la Israel jana Jumamosi, watu waishio katikati mwa Rafah walishauriwa kuhama. Jumatatu iliyopita, jeshi la Israel lilitoa taarifa likiwashauri watu wa mashariki mwa Rafah kuhama.

Jana Jumamosi, vyombo vya habari vya Palestina viliripoti kwamba Wapalestina saba waliuawa kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel huko Rafah.

Mamlaka za afya kwenye ukanda huo zilitangaza kwamba watu 34,971 wameuawa huko Gaza tangu mgogoro ulipoanza.