Urusi yasema vikosi vyake ilivitwaa vijiji vitano vilivyopo Kharkiv mashariki mwa Ukraine

Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema vikosi vyake vimevitwaa vijiji vitano kwenye eneo la Kharkiv mashariki mwa Ukraine.

Vikosi vya ardhini vya Urusi vilivuka mpaka kutoka kaskazini na kuingia Kharkiv juzi Ijumaa huku vikifanya mashambulizi makubwa ya mabomu.

Gavana wa Kharkiv Oleh Syniehubov alisema jana Jumamosi kwamba mapigano makali yamelazimisha wakazi karibu 2,000 kuhama. Alidai kwamba vikosi vya Ukraine vimevizuia vikosi vya Urusi kusonga mbele.

Katika ujumbe wa video uliotolewa juzi ijumaa, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine alisema serikali yake inatuma wanajeshi zaidi kuelekea Kharkiv. Alisema jaribio lolote la uvamizi la Urusi, litazuiwa.

Jeshi la Ukraine lilisema jana Jumamosi kwamba mapigano makali dhidi ya vikosi vya Urusi yaliendelea kwenye eneo la mashariki la Donetsk na kwingineko.

Taasisi ya Utafiti wa Vita ya Marekani inayotoa ushauri wa kitaalam, juzi Ijumaa ilitoa ripoti ya tathmini yake inayosema “Kuna uwezekano mkubwa vikosi vya Urusi kuboresha mwelekeo wao wa kimbinu huko kaskazini mwa Kharkiv katika siku zijazo ili kuongeza operesheni ya mashambulizi.”

Ripoti hiyo iliongeza kwamba “Operesheni za mashambulizi za Urusi kwenye mpaka wa kimataifa wa Kharkiv yanaweza kuwa na lengo la kimkakati la kuvivuta na kuvifunga vikosi vya Ukraine katika eneo hilo kuwezesha Warusi kusonga mbele katika maeneo mengine ya mashariki mwa Ukraine.”