Mashirika ya UN yatoa tahadhari juu ya msaada kwa ukanda wa Gaza

Wapatanishi wanaojaribu kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano katika mgogoro kati ya Israel na kundi la Hamas wamesitisha majadiliano yao. Hata hivyo, maafisa wa misaada wa Umoja wa Mataifa UN wameonya jana Ijumaa kwenye mkutano na wanahabari kwamba “ni usitishaji mapigano pekee” utakaoepusha umwagaji damu zaidi na uthabiti unaohitajika sana ili kufikisha misaada.

Afisa wa Ofisi ya UN ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu Georgios Petropoulos alisema mashambulizi ya mabomu ya Israel yameendelea “kote katika eneo la Rafah.” Aliongeza kwamba kundi lake pia linashuhudia mashambulizi yanayofanyika “yakiongezeka karibu kabisa na Muwasi,” ambalo ni eneo vikosi vya Israel vimelitenga kama “ukanda wa kibinadamu.”

Maafisa wa UN wanasema mamia kwa maelfu ya watu waliopoteza makazi yao wanajihifadhi hapo, lakini shughuli za kijeshi za Israel zinawazuia kuwasilisha misaada katika njia “inayoonekana" na "salama.”

Maafisa walisema hakuna lori lililoweza kuingia ukanda wa Gaza tangu vikosi vya Israel vilipodhibiti mpaka wa Rafah mapema juma hili, hivyo wamekuwa “wakijaribu kuokoteza kwenye maghala” kwa chakula na mafuta.