Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wafufua maombi ya Palestina kuwa mwanachama

Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, UN umepitisha kwa kishindo azimio linalounga mkono ombi la Palestina kuwa mwanachama kamili wa UN. Umependekeza kwamba Baraza la Usalama liangalie upya suala hilo “kwa upendeleo.”

Azimio hilo lilipitishwa jana Ijumaa kwa kura 143 zilizounga mkono na tisa zikipinga, zikiwemo za Marekani na Israel. Nchi 25 hazikupiga kura.

Wajumbe wa mkutano huo walishangilia kwa kupiga makofi azimio hilo lililopopitishwa, na waliunda mstari kukumbatiana na Balozi wa Palestina UN, Riyad Mansour.

Kwa sasa Wapalestina wana hadhi ya mwangalizi asiye mwanachama. Azimio hilo linawatambua kama waliokidhi kujiunga kwa ukamilifu.

Uanachama kamili unahitaji pendekezo kutoka Baraza la Usalama la UN. Hata hivyo, ujumbe wa Marekani ulipinga pendekezo hilo kwa kura ya turufu mwezi uliopita.