Wataalam wa hali ya hewa: milipuko ya miako ya Jua huenda ikavuruga mawasiliano

Wataalam wa hali ya anga za juu wanasema milipuko ya miako ya jua yenye nguvu katika siku kadhaa zijazo inaweza kuvuruga satelaiti za mawasiliano, GPS na redio za mawimbi ya masafa mafupi kote duniani.

Milipuko ya jua, ama utoaji mkubwa wa korona ni uondoaji wa plazma na uga wa sumaku kutoka sehemu ya anga hewa la Jua.

Mamlaka ya Taifa ya Bahari na Anga ya Marekani ilisema miako inasababisha dhoruba ya sumaku ardhini inayoweza kudumu hadi leo Jumapili. Imetoa hadhari ya pili ya kiwango cha juu kwa ajili ya kutokea kwa dhoruba kama hiyo.

Taasisi ya taifa ya Japani ya Taarifa na Mawasiliano inasema miako haiwezi ikaathiri huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi. Lakini ilionya kwamba GPS na aina fulani ya mawasiliano ya redio huenda yakaathirika katika siku zijazo.

Moja ya athari ya miako hiyo ni kwamba ‘Northern Lights’ inaweza kuonekana katika latitudo ya chini kuliko kawaida. Watu kote duniani wamekuwa wakichukua picha za rangi za kupendeza katika maeneo yao.