Maandamano yazuka kupinga ushiriki wa Israel kwenye shindano la wimbo bora la Eurovision

Usalama umeimarishwa kwenye ukumbi wa Shindano la Wimbo Bora la Eurovision nchini Uswidi kufuatia upinzani wa ushiriki wa Israel.

Mwimbaji wa Israel Eden Golan amefanikiwa kuingia fainali inayofanyika leo Jumamosi, mwaka huu likifanyikia mjini Malmo nchini Uswidi.

Tukio hilo ni shindano kubwa kabisa la muziki barani Ulaya.

Shirika la habari la Uingereza, Reuters linasema maelfu ya watu walikusanyika mjini humo juzi Alhamisi kupinga mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza. Waliripotiwa kuungana na mwanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi, Greta Thunberg.

Waandamanaji walibeba mabango yaliyoandikwa, “Acha kutumia Eurovision kuficha uhalifu wa Israel.”

Mwandamanaji mmoja alisema waandaaji wa shindano hilo walipaswa kuiondoa Israel, kama walivyofanya kwa Urusi wakati wa uvamizi wa Ukraine. Alisema, “Siyo kweli kwamba Eurovision si ya kisiasa.”

Mwimbaji wa Israel aliwaambia wanahabari kuwa ni heshima kuiwakilisha nchi yake.