Miako mikali ya Jua inaweza kutatiza mawasiliano na GPS

Watafiti wa hali ya hewa ya anga la juu wanasema mfululizo wa miako mikali ya Jua inaweza kutatiza satelaiti za mawasiliano, GPS na redio ya mawimbi mafupi duniani kote katika siku chache zijazo.

Miako hiyo ya Jua ni milipuko mikubwa ya mionzi ya sumaku umeme kutoka kwenye Jua. Inaweza kuathiri Dunia kwa wingi wa mionzi ya protoni zilizotolewa na chembe nyingine zenye chaji.

Maafisa wa Taasisi ya Kitaifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Japani wanasema miako ya Jua mikali zaidi ilishuhudiwa mara tano kati ya Jumatano na mapema jana Ijumaa kwa saa za Japani.

Wanasema dhoruba hiyo ya usumaku wa kijiografia inaweza kufikia Dunia mapema jana Ijumaa usiku.