Netanyahu aapa kuendelea na operesheni mjini Rafah

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema “hakuna kiwango chochote cha shinikizo,” ambacho kitaisimamisha nchi hiyo dhidi ya kujilinda yenyewe. Aliyasema hayo kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani Joe Biden kusitisha usafirishaji wa silaha nchini mwake. Alisema jana Alhamisi kuwa ikiwa Israel lazima “isimame peke yake,” itafanya hivyo.

Netanyahu ameshuhudia vikosi vyake vikimaliza nyingi ya silaha zake wakati vikishambulia kwa mabomu baadhi ya maeneo ya mji wa Rafah. Alisema kuwa, ikiwa lazima, vitapigana kwa kutumia “kucha” zao.

Wapatanishi wa Israel wamejiondoa kwenye mazungumzo ya kusitisha vita mjini Cairo nchini Misri. Viongozi wa Hamas walitoa taarifa jana Alhamisi wakisema wajumbe wao pia wameondoka. Walisema uvamizi wa mji wa Rafah “unalenga kuzuia jitihada za wapatanishi.”

Msemaji wa usalama wa taifa wa Ikulu ya Marekani John Kirby ameonya kuwa operesheni kubwa ya ardhini “kwa kweli itaimarisha” Hamas kwenye meza ya mazungumzo. Aliongeza kuwa Marekani inafanya kazi na Israel kutafuta njia mbadala ya kuondoa matishio badala ya “kuvamia Rafah.”