Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani ajibu matamshi ya Seneta wa Marekani kuhusu mashambulizi ya mabomu ya atomiki

Waziri wa mambo ya nje wa Japani amejibu mjadala katika Bunge la Seneti la Marekani uliogusia shambulio la mabomu ya atomiki katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japani. Matamshi ya mashambulizi hayo yaliibulika wakati wa mjadala kuhusu uungaji mkono kijeshi wa Marekani kwa Israel katika mapambano yake dhidi ya kundi la Hamas.

Matamshi hayo yaliibuka wakati wa kusikilizwa kwa kamati ndogo ya Seneti siku ya Jumatano wiki hii iliyohusisha kusimamishwa kwa sehemu ya usafirishaji wa silaha za Marekani. Seneta wa chama cha Republican Lindsey Graham amehimiza uwasilishaji wa silaha uanze tena, akirejelea mashambulizi ya mabomu ya atomiki ya mwaka 1945.

Graham alisema: "Wape Israeli kile wanachohitaji kupigana vita ambavyo hawawezi kumudu kupoteza. Hii ni Hiroshima na Nagasaki kwa ukubwa zaidi."

Wakati fulani, Graham aliwashinikiza maafisa wakuu wa ulinzi wa Marekani iwapo walifikiri matumizi ya silaha za nyuklia yalikuwa ya haki.

Graham aliuliza, "Kwa mtazamo wa nyuma unafikiri huo ulikuwa uamuzi sahihi kwa Marekani kudondosha mabomu mawili ya atomiki kwenye miji husika ya Japani?"

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Marekani, Jenerali Charles Q. Brown alijibu, "Nitakuambia ilisimamisha vita vya dunia."

Graham kisha akamwuliza Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin: "Je, unakubali Jenerali Austin? Ikiwa ungekuwepo, ungesema wadondoshe hayo mabomu?"

Austin akajibu, "Nakubaliana na Mwenyekiti hapa."

Jana Ijumaa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Kamikawa Yoko aliulizwa maoni yake juu ya matamshi hayo na mwana habari.

Alisema: "Ninaamini matamshi hayo kuhusu Hiroshima na Nagasaki hayakufaa. Japani inafahamu kwamba milipuko ya mabomu ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki iligharimu maisha ya watu wengi sana na kusababisha hali ya kusikitisha ya kibinadamu ambapo watu walipata shida zisizoelezeka kutokana na magonjwa na ulemavu."

Kamikawa aliongeza kuwa: "Kama serikali imekuwa ikisema kwa muda mrefu, tunaamini kwamba matumizi ya silaha za nyuklia hayalingani na utu wa ubinadamu, ambao ni msingi wa kiitikadi wa sheria za kimataifa, kwa sababu ya nguvu zao kubwa za uharibifu na hatari. "

Kamikawa alisema Japani iliwasilisha maoni hayo kwa Marekani, na pia kwa ofisi ya Seneta Graham.