Ofisi ya UNRWA Yerusalemu Mashariki kufungwa kufuatia madai ya uchomaji moto

Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu, UNRWA linasema litafunga ofisi ya makao makuu yake yaliyopo Yerusalemu Mashariki hadi usalama thabiti utakaporejeshwa. UNRWA inasema wakazi wa Israel walichoma moto mara mbili eneo linalozunguka ofisi hiyo juzi Alhamisi.

Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini alitoa tangazo hilo kwenye mtandao wa X, zamani ukijulikana kama Twitter.

Alisema kwamba licha ya kutokuwepo waathirika miongoni mwa wafanyakazi wa ofisi za makao makuu, walilazimika kuzima moto wao wenyewe kwani ilichukua muda kwa mamlaka za zimamoto za Israel kufika kwenye eneo la tukio. Aliongeza kwamba ofisi hiyo ina vituo vya petroli na dizeli kwenye eneo lake kwa ajili ya magari ya shirika hilo.

Lazzarini aligusia kwamba serikali ya Israel ina jukumu la kuhakikisha kuwa maafisa wa UN na vituo vyake vinalindwa wakati wote na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi.