Mwenge wa Mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 waanza kukimbizwa kote nchini Ufaransa

Ukimbizaji wa mwenge wa Mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 ulianza jana Alhamisi katika jiji la Marseille, kusini mwa Ufaransa chini ya ulinzi mkali.

Mwenge huo uliwasili jijini humo ukitokea nchini Ugiriki siku iliyotangulia.

Mkimbizaji wa kwanza wa mwenge huo alikuwa ni Basile Boli ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya Ufaransa.

Chini ya mbingu safi ya bluu, makundi makubwa ya watu walijitokeza na kushangilia kwenye njia mwenge huo ulipokuwa ukipitishwa.

Makumi ya maafisa wa polisi yaliwasindikiza wakimbiaji kwa miguu na pikipiki.

Mwenge huo utakimbizwa na wakimbiaji karibu 10,000. Hatimaye utawasili kwenye Mto Seine kwa ajii ya hafla ya ufunguzi Julai 26 mwaka huu.