Waziri Mkuu wa Japani apanga kuhudhuria mkutano wa amani kuhusu Ukraine nchini Uswizi

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio anapanga kuhudhuria mkutano wa kimataifa nchini Uswizi mwezi ujao ili kujadili mchakato wa amani wa Ukraine. Hii ni kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya serikali.

Kishida anatarajiwa kuahidi kwamba Japani itaendelea kutoa msaada kwa Ukraine na kuthibitisha umoja wa mataifa ambayo yana matumaini ya kufikiwa kwa amani.

Serikali ya Uswizi ilitangaza mapema mwezi huu kwamba itaandaa Mkutano wa Amani wa Viongozi Wakuu juu ya Ukraine utakaofanyika katika eneo la kitalii la Burgenstock Juni 15 na 16 mwaka huu.

Ilisema wahudhuriaji watajadili mpango wa amani ulioandaliwa na Ukraine na mapendekezo mengine. Ukraine imependekeza mpango wa amani wenye hoja kumi unaojumuisha kuondolewa kwa vikosi vya Urusi na kurejeshwa kwa uadilifu wa eneo la Ukraine.

Serikali ya Uswizi ilisema imewaalika wajumbe zaidi ya 160 kutoka kote duniani.

Katika mkutano huo, Kishida anatarajiwa kusisitiza ahadi za Japani zisizoyumba katika kuisaidia UKraine na kudumisha vikwazo dhidi ya Urusi.

Kabla ya ziara yake nchini Uswizi, Kishida anapanga kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizostawi zaidi kiviwanda duniani uliopangwa kuanza Juni 13 nchini Italia.