Viongozi wa China na Hungary wakubaliana kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Rais wa China Xi Jinping na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban wamekubaliana kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili kupitia mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja.

Xi alikutana na Orban jana Alhamisi nchini Hungary, ikiwa ni sehemu ya mwisho katika ziara yake barani Ulaya baada ya kuzuru Ufaransa na Serbia.

Hungary imeweka umuhimu kwenye uhusiano wake na China. Ingawa Umoja wa Ulaya, EU unatafuta “kupunguza hatari” ya uhusiano na China kwa kupunguza utegemezi wa kiuchumi kupita kiasi, Hungary ambayo ni mwanachama wa umoja huo inazidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na China.

Viongozi hao wawili wameripotiwa kukubaliana kuendelea na ujenzi wa reli inayounganisha Hungary na Serbia chini ya mpango wa Ukanda Mmoja Njia Moja. Pia walithibitisha kuwa mataifa hayo mawili yataimarisha uhusiano kupitia uwekezaji wa makampuni ya China.

Baada ya mkutano wao, Orban aliwaambia wanahabari kuwa ulimwengu kwa sasa una nchi nyingi zenye nguvu, na kwamba moja ya mihimili ya utaratibu huu mpya duniani ni China.

Waziri huyo mkuu wa Hungary pia alielezea utayari wake katika kupanua ushirikiano na China katika nyanja ya uzalishaji wa umeme wa nyuklia.

Hungary inatarajiwa kupokea urais wa zamu wa EU katika nusu ya pili ya mwaka huu.

Waangalizi wa mambo wanasema Rais Xi anajaribu kuongeza mivutano kati ya nchi wanachama wa EU kwa kuimarisha uhusiano wake na Hungary.