Taiwan yasema meli 11 za China zimeingia katika bahari zilizopo jirani na Visiwa vya Kinmen

Taiwan inasema kuwa meli 11 za serikali ya China zimeingia katika bahari zilizopo jirani na Visiwa vya Kinmen. Taiwan inavidhibiti visiwa hivyo na inazielezea bahari zilizo karibu na visiwa hivyo kama “zilizozuiwa” na “zilizokatazwa.” Inazizuia meli za China kuingia katika bahari hizi bila kibali.

Kikosi cha walinzi wa pwani cha Taiwan kinasema meli saba za serikali ya China, ikiwa ni pamoja na meli za masuala ya bahari na za uvuvi, ziliingia bila kibali katika bahari zinazozuiwa majira ya saa tisa alasiri jana Alhamisi.

Kinasema meli nne za walinzi wa pwani wa China pia ziliingia katika bahari zilizozuiwa na zilizokatazwa karibu muda huo huo.

Kikosi cha Walinzi wa Pwani cha Taiwan kinasema meli 11 zilisalia katika bahari hizo kwa takribani dakika 90 licha ya boti za doria kutoa onyo la kuzitaka kuondoka.

Kinasema hii ni mara ya nne mwezi huu kwa meli za Kikosi cha Walinzi wa Pwani cha China kusafiri kwa mpangilio katika eneo hilo. Kinaongeza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa meli za Kikosi cha Walinzi wa Pwani cha China kuungana na meli za taasisi zingine za serikali katika kuingia katika bahari hizo.

Mwezi Februari mwaka huu, wavuvi wawili wa China walifariki baada ya boti yao kuzama wakati wakifuatwa na walinzi wa pwani wa Taiwan katika bahari zilizopo jirani na Visiwa vya Kinmen. China ilijibu kwa kusema hakuna bahari zilizozuiwa au kukatazwa.

Wachambuzi wanasema China inajaribu kuongeza shinikizo kwa utawala wa Rais wa Taiwan Lai Ching-te ambaye anatarajiwa kuingia madarakani Mei 20 mwaka huu.