Wizara ya Ulinzi ya Japani yasema video ya manowari ya SDF huenda ni ya kweli

Wizara ya Ulinzi ya Japani imethibitisha kwamba video ambayo ni dhahiri ni ya manowari ya Kikosi cha Kujihami cha Majini, MSDF ambayo inaonekana ilichukuliwa na droni isiyoidhinishwa yawezekana ni ya kweli.

Video hiyo iliwekwa kwenye tovuti ya kushirikishana picha za video ya China mwezi Machi. Inaonekana kuonyesha manowari ya Izumo ikiwa imetia nanga kwenye kambi ya MSDF mjini Yokosuka, kusini mwa Tokyo.

Wizara hiyo ilisema jana Alhamisi kwamba video hiyo inawezekana ni ya kweli.

Safari zisizoidhinishwa za ndege zisizokuwa na rubani jirani na juu ya kambi za SDF zimepigwa marufuku kisheria.

Wizara ilikataa kubainisha iwapo safari ya droni inayoshukiwa ilikuwa imetambuliwa. Imeelezea wasiwasi kwamba kufichua taarifa kama hizo kunaweza kuhatarisha uwezo wa kiusalama wa SDF.

Wizara hiyo imeahidi kufanya kila iwezalo kuongeza uwezo wake wa usalama, ikiwemo kutambulisha mapema vifaa vya kisasa zaidi vinavyoweza kutambua droni.