Waziri wa Ulinzi wa Marekani athibitisha kusitishwa kwa msaada wa kijeshi kwa Israel

Rais wa Marekani Joe Biden ameamua kusitisha usafirishaji wa shehena ya silaha kwenda Israel. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amethibitisha uamuzi huo jana Jumatano kwenye mkutano wa Kamati ya Mipango ya Seneti.

Austin aliwahakikishia wabunge kwamba dhamiri ya Marekani katika usalama wa Israel ipo “imara.” Hata hivyo, alisema utawala wa Biden “unapitia tena” msaada huo kutokana na “matukio yanayoendelea” huko Gaza. Aliongeza kwamba Israel haipaswi kuanzisha shambulio kubwa huko Rafah “pasipo kuzingatia na kuwalinda raia waliopo katika eneo hilo la vita.”

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alizungumzia suala hilo kwenye mkutano. Alisema usaidizi wa Marekani tangu kuanza kwa mgogoro huo mwezi Oktoba mwaka jana umekuwa katika kiwango “kisicho na kifani.” Aliongeza kwamba “mizozo” yoyote inatatuliwa kwa njia ya “faragha.”

Wapatanishi kutoka Israel na Hamas wanapima mapendekezo ya hivi karibuni kwa ajili ya kusitisha mapigano. Hazijatolewa ripoti zozote kuhusu maendeleo yaliyofikiwa.

Vikosi vya Israel vilitwaa udhibiti wa mpaka ulio muhimu kwa ajili ya kupeleka msaada wa kibinadamu na imeufunga tangu wakati huo.

Vikosi hivyo vinasema vimefungua tena mpaka mwingine huko Kerem Shalom kuruhusu misaada kusafirishwa kwenda Gaza. Lakini, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew MIller alisema kiwango cha misaada ya kibinadamu “hakikubaliki” na kwamba Rais Biden amekuwa akimweleza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa kunahitajika kuwepo “mabadiliko makubwa.”
###