Rais wa China ajadili juu ya “mustakabali wa pamoja” na Serbia

Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Serbia Aleksander Vucic wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao ili kujenga “mustakabali wa pamoja.”

Xi alikutana na Vucic jana Jumatano katika mji mkuu wa Serbia, Belgrade. Hiki ni kituo cha pili katika ziara ya Rais Xi kwenye mataifa ya barani Ulaya.

Viongozi hao wawili walitia saini makubaliano ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi na mabadilishano ya wafanyakazi.

Xi alielezea kuiunga mkono Serbia juu ya msimamo wake kuhusu Kosovo, iliyojitangazia uhuru kutoka Serbia mwaka 2008. Alisema anaunga mkono jitihada za Serbia za kulinda uadilifu wa eneo lake.

Vucic aliunga mkono msimamo wa China unaoionaTaiwan kama sehemu ya China.

Xi aliwasili hapo katika tarehe muhimu ya kumbukumbu ya mwaka wa 25 ya shambulio lisilokusudiwa lililofanywa na majeshi NATO kwenye ubalozi wa China katika iliyokuwa Yugoslavia. Marekani iliiongoza kampeni ya kijeshi ya vikosi vya umoja huo.

Xi aliandika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la kila siku la Serbia akisema watu wa China “hawataruhusu kamwe historia mbaya kama hiyo ijirudie.”
###