Hakuna ongezeko la mshahara kwa wafanyakazi wengi vibarua katika mazungumzo ya msimu wa chipukizi nchini Japani

Kundi la wafanyakazi vibarua wanaotazamia kuongezwa mshahara nchini Japani linasema karibu nusu ya makampuni husika hayajakubali matakwa yao katika mazungumzo ya mshahara ya msimu wa chipukizi.

Kwenye mkutano na wanahabari jana Alhamisi, kundi hilo lilisema kwamba takribani wafanyakazi 30,000 walitaka nyongeza ya mshahara ya asilimia 10 ama zaidi kutoka kwa waajiri 107. Asilimia 55 ya makampuni yamejibu hadi kufikia sasa.

Lakini kundi hilo limesema wastani wa ongezeko la mshahara huo ni asilimia 3 hadi 4 tu, na makampuni 48 yaliyosalia bado hayajakubali kuongeza mshahara.

Kundi hilo pia lilielezea kwamba karibu asilimia 70 ya waajiri waliojibu kwenye utafiti wa wafanyakazi wa muda na vibarua uliofanyika mwezi huu walisema hawataongeza mshahara kabisa.

Kundi hilo linasema si kawaida kwa wafanyakazi vibarua kupigania na kufanikiwa kuongezewa mshahara, na wataendelea na mazungumzo hayo kwani matokeo yamekuwa madogo hadi sasa.

Kulikuwa na zaidi ya wafanyakazi vibarua milioni 21 nchini Japani mwaka jana ambao ni asilimia 37 ya nguvu kazi ya nchi hiyo.