Mishahara halisi nchini Japani yaendelea kushuka

Takwimu za hivi karibuni za serikali zinaonyesha mfumuko wa bei unaendelea kuathiri mishahara ya watu nchini Japani.

Wizara ya kazi ya nchi hiyo inasema mfumuko umeongeza kushuka kwa thamani ya mishahara kwa asilimia 2.5 katika mwezi wa Machi kulinganisha na mwezi kama huo mwaka jana. Huo ulikuwa ni mwezi wa 24 mfululizo wa kushuka.

Takwimu hizo zinatokana na utafiti wa kila mwezi wa biashara zaidi ya 30,000 zenye wafanyakazi wasiopungua watano.

Wastani wa mshahara wa kawaida kwa mwezi Machi ulipanda kwa asilimia 0.6 hadi zaidi ya yen 301,000, ama karibu dola 1,940. Hiyo inafanya mwezi wa 27 mfululizo wa kuongezeka.

Wizara hiyo inasema idadi ya waajiri kwa mwaka 2024 wanaoongeza mishahara kwa wafanyakazi wao inatarajiwa kuongezeka kutoka mwaka jana. Mwenendo huo unaonyesha matokeo ya majadiliano ya kila mwaka kati ya kampuni kubwa na vyama vya wafayakazi.
###