Wanafunzi katika vyuo vikuu zaidi ya 10 vya Uingereza waandamana dhidi ya Israel

Maandamano ya kupinga mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza yameandaliwa katika vyuo vikuu zaidi ya 10 vya Uingereza huku maandamano katika vyuo vikuu nchini Marekani yakiendelea, na waandamanaji wengi wakikamatwa.

Wanafunzi na wafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Cambridge wameweka kambi ya karibu mahema 50.

Waandamanaji hao wanakitaka chuo kikuu hicho kuacha kuwekeza katika kampuni zinazosambaza silaha kwa Israel. Pia wanasema haipaswi kukubali ufadhili wa utafiti kutoka kwa kampuni kama hizo.

Mwanafunzi mmoja alisema wanalenga kuhakikisha kuwa ada yao ya masomo haitumiki kwa jambo ambalo hawakubaliani nalo. Aliongeza kuwa maandamano yataendelea hadi chuo kitakaposikiliza matakwa yao.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak aliambia kikao cha Baraza la Mawaziri juzi Jumanne kwamba kumekuwa na "ongezeko lisilokubalika" la chuki dhidi ya Wayahudi kwenye vyuo vikuu.

Sunak anatarajiwa kutoa wito kwa makamu wa vyuo vikuu kutumia mbinu thabiti kwa tabia isiyokubalika katika mkutano kwenye ofisi ya waziri mkuu leo Alhamisi.
###