Idadi ya waliofariki kutokana na mvua kubwa iliyonyesha nchini Brazil yaongezeka hadi 100

Mamlaka kusini mwa Brazil inasema idadi ya waliofariki kutokana na mvua kubwa imeongezeka hadi 100. Uporaji umeripotiwa katika maeneo yaliyoathiriwa na hivyo kuzua wasiwasi wa kiusalama.

Mvua kubwa iliyoanza kunyesha mwishoni mwa mwezi Aprili imesababisha mafuriko makubwa katika jimbo la Rio Grande do Sul.

Maafisa wa eneo hilo walisema jana Jumatano kuwa watu 100 wamethibitishwa kupoteza maisha na wengine 128 hawajulikani walipo.

Maafa hayo yameripotiwa kulazimisha zaidi ya watu 160,000 kuhama, na watu milioni 1.45 wameathiriwa, ikiwa ni pamoja na kukatika kwa umeme na maji.

Vyombo vya habari nchini humo vinasema kulikuwa na ripoti za uporaji katika maduka na nyumba na wizi wa boti za kuokoa maisha.

Jimbo la Rio Grande do Sul ni mzalishaji mkubwa wa nafaka nchini Brazil, likichangia asilimia 70 ya uzalishaji wa mpunga nchini humo.

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amesema nchi hiyo itaagiza mchele na bidhaa zingine kama zikihitajika.
###