Uingereza kumfukuza mwambata wa jeshi wa Urusi ikidai ni “jasusi wa kimyakimya’

Uingereza imesema itamfukuza mwambata wa kijeshi wa Urusi kutoka nchini humo, ikidai mtu huyo ni Afisa wa ujasusi wa kimyakimya.

Serikali ya Uingereza jana Jumatano imetangaza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya hatua dhidi ya kile ilichosema ni “vitendo viovu” vya Urusi nchini Uingereza.

Serikali hiyo pia imesema itaondoa hadhi ya diplomasia kwenye mali kadhaa za Urusi nchini Uingereza. Imesema zinaaminika kutumika kwa madhumuni ya kijasusi.

Hatua nyingine ni kupunguza muda wa wanadiplomasia wa Urusi kukaa nchini Uingereza.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza James Cleverly amesema serikali “Inachukua hatua ya kutuma ujumbe mkali kwa Urusi na kupunguza zaidi uwezo” wa Shirika la kijasusi la nchi hiyo.

Nchini Uingereza, raia sita wa Bulgaria wameshtakiwa tangu mwaka jana kwa kosa la ujasusi kwa Urusi. Serikali ya Uingereza inaona kuwa idadi ya mashambulizi ya mtandaoni yanayolenga wabunge wa Uingereza na wengineo katika miaka ya hivi karibuni yalifanywa na Urusi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova katika taarifa ya mtandaoni jana Jumatano amesema kwamba Urusi imeonya kuwa itajibu vitendo visivyo rafiki. Ameongeza kuwa jibizo hilo litakuwa kali.
###