Serikali ya Japani: 15% ya wazee Japani watakuwa na dementia ifikapo mwaka 2040

Wizara ya afya ya Japani inaonya juu ya ongezeko la shida ya kupoteza kumbukumbu yaani dementia linalokuja. Maafisa wanakadiria kuwa kufikia mwaka wa 2040 wazee zaidi ya milioni 5.8 watakuwa na hali hiyo ambapo ni takriban asilimia 15 ya jumla ya wazee wote.

Watafiti wa wizara hiyo walizingatia makadirio ya kuenea kwa dementia miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 65 au zaidi katika manispaa nne nchini humo.

Wanasema idadi ya wazee walio na shida hiyo itaongezeka kwa zaidi ya milioni 1.1 katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

Zaidi ya hayo, wanasema zaidi ya watu milioni 6.1 watakuwa na shida kidogo ya utambuzi, MCI kufikia mwaka 2040. Watu wenye MCI wanapoteza kumbukumbu lakini haiathiri sana maisha yao ya kila siku. Ijapokuwa, mara nyingi husababisha dementia.

Wengi kati ya wale walio na dementia watakuwa wakiishi peke yao. Mtaalamu mmoja anasisitiza haja ya usaidizi wa jamii.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Toyo Takano Tatsuaki anasema jamii kwa ujumla italazimika kukubaliana kuweka mifumo ya msaada kwa watu wenye dementia.

Anaonya kuwa hakutakuwa na wataalamu wa kutosha kumuhudumia kila mtu.
###