Vikosi vya Israel vyauteka mpaka wa Rafah

Viongozi wa Israel wamepeleka wanajeshi katika mji wa Rafah uliopo kusini mwa Gaza licha ya wito kutoka kote duniani wa kujizuia kufanya oparesheni ya ardhini.

Jana Jumanne, vikosi vya nchi hiyo vilichukua udhibiti wa mpaka muhimu wa kuwasilisha misaada.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema kuuteka mpaka huo ni “hatua muhimu” ya kuharibu “uwezo wa kijeshi uliosalia wa Hamas.”

Kuhusu pendekezo la hivi karibuni la kusitisha mapigano, Netanyahu alisema lipo “mbali” na “mahitaji muhimu” ya Israel. Ametuma ujumbe jijini Cairo ili “kusimamia imara” masharti hayo.

Viongozi wa Hamas pia wamepeleka wawakilishi. Walisema “kuutwaa” mpaka wa Rafah ni kosa kubwa la kihalifu na kuonya kwamba, ikiwa “uvamizi” huo utaendelea, hakutakuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano.

Msemaji wa usalama wa taifa wa Ikulu ya Marekani John Kirby alisema oparesheni hiyo si ya kushambulia ambayo Marekani ilikuwa ikionya. Aliongeza kuwa Israel imeielezea oparesheni hiyo kama moja “yenye ukomo wa wigo, ukubwa na muda.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema mashambulizi kamili yatakuwa ni “makosa ya kimkakati” na “tatizo kubwa la kibinadamu.” Maafisa wengine wa Umoja wa Mataifa wanasema utekaji wa mpaka huo “umekwamisha” misaada kwa Gaza na kwamba mpaka mwingine muhimu wa Kerem Shalom bado umefungwa.
###