Ukraine yazuia njama ya kumuua Zelenskyy

Idara ya usalama ya Ukraine ilitangaza jana Jumanne kwamba imezuia njama ya kumuua Rais Volodymyr Zelenskyy. Ilisema imewaweka kizuizini maafisa wawili waandamizi wa Ukraine na kuwashutumu kwa kufanya kazi kwa niaba ya Urusi.

Wachunguzi walisema watu hao walikuwa makanali katika kikosi cha ulinzi wa taifa na kwamba wamekamatwa kwa tuhuma za uhaini.

Idara ya usalama pia ilisema kuwa njama hiyo ni pamoja na kumuua kiongozi wa idara hiyo, Vasyl Maliuk, na mkuu wa ujasusi wa kijeshi, Kyrylo Budanov.

Ilisema washukiwa hao walipaswa kufuatilia mienendo ya walengwa wao kabla ya kutuma taarifa hizo kwa Warusi. Mpango ulikuwa kufuatisha mashambulizi ya makombora na droni.
###