Vyombo vya habari vinasema Marekani yasitisha kwa kiasi fulani usafirishaji wa silaha kwenda Israel

Vyombo vingi vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden umesitisha kwa kiasi fulani usafirishaji wa silaha kwenda Israel.

Tovuti ya habari za kisiasa ya Politico ilisema uwasilishaji wa aina mbili za mabomu yanayolenga shabaha kwa usahihi umesitishwa. Iliripoti, "Hii inaonekana kuwa ni mara ya kwanza kwa utawala wa
Marekani kuchelewesha uwezekano wa kuiuzia Israel silaha" tangu shambulio la Hamas dhidi ya nchi hiyo mwezi Oktoba mwaka jana.

Tovuti hiyo ya habari ilimnukuu afisa wa Marekani akisema kuwa kusitishwa kwa usafirishaji wa silaha kunalenga kutuma "ujumbe wa kisiasa kwa Israel."

Marekani imeendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Israel. Lakini inaitaka Israel kuwalinda raia huku kukiwa na ukosoaji unaoongezeka ndani na nje ya nchi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya raia katika Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Marekani John Kirby alisema jana Jumanne kuwa hazungumzii kuhusu shehena moja moja za msaada wa kijeshi wa Marekani, lakini hakuna kilichobadilika kuhusu dhamira ya Marekani kwa usalama wa Israel.
###