Afisa wa UN apata wasiwasi mkubwa kuhusu silaha za AI

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Upokonyaji wa Silaha amesema Umoja wa Mataifa unataka kujenga uelewa kuhusu madhara ya matumizi ya kijeshi ya teknolojia ya akili komputa, AI. Afisa huyo anatumai kuwa uelewa huo utaongeza kasi ya mazungumzo kuhusiana na umuhimu wa taratibu za kimataifa.

Naibu Katibu Mkuu na Mwakilishi kwa Masuala ya Upunguzaji Silaha Nakamatsu Izumi alihojiwa na NHK. Silaha zinazotumia AI zimeripotiwa kutumika katika Ukanda wa Gaza na Ukraine.

Nakamatsu alisema anahisi hali ya hatari, kadri silaha zinazotumia teknolojia ya AI zinavyoendelea kutengenezwa ili zitumike wakati wa vita. Alisema ana wasiwasi kwamba shiraha hizo zitaleta mabadiliko makubwa katika namna vita vinavyoongozwa na kupiganwa.

Wasiwasi unazidi kuongezeka kuhusu Mifumo ya Silaha Kali Zinazojiendesha zenyewe, LAWS. Mifumo ya silaha hizo inachagua na kushambulia maeneo lengwa bila usimamizi wa binadamu.

Mwaka jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito kwa nchi wanachama kuidhinisha mpango kazi wa kisheria wa LAWS ifikapo mwaka 2026, kwa kuwa kwa sasa hakuna sheria za kimataifa zinazodhibiti mifumo hiyo.

Kuhusu suala hilo, Nakamatsu alirejelea pengo kati ya mataifa ambayo tayari yanaendeleza teknolojia hiyo na yale ambayo hayaendelezi. Alisema mataifa makubwa kijeshi yanajaribu kuongoza katika utengenezaji wa LAWS. Aliongeza kuwa mataifa hayo yanataka kujinufaisha katika majadiliano.

Pia aligusia uwezekano ambao magaidi na taasisi zingine zinavyoweza kutumia vibaya AI.

Alisisitiza kuwa ni muhimu kuyafanya mataifa na watu wote kuelewa kwamba matumizi mabaya ya AI yanaweza kuleta madhara makubwa.###