Japani, China na Korea Kusini zajiandaa kufanya mkutano wa viongozi wakuu mwishoni mwa Mei

Japani, China na Korea Kusini zinafanya maandalizi ya kufanya mkutano wa viongozi wakuu wa nchi hizo tatu mwishoni mwa mwezi huu. Itakuwa ni mara ya kwanza kufanyika kwa mkutano kama huo katika kipindi cha takribani miaka minne na nusu.

Vyanzo vya habari vya serikali vinasema Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio, Waziri Mkuu wa China Li Qiang na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol wamepanga kukutana jijini Seoul nchini Korea Kusini. Kishida huenda akatembelea Korea Kusini kuanzia Mei 26 hadi 27.

Japani inatafuta kufikia makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na
mabadilishano ya watu katika hatua ya kuhamasisha amani na uthabiti barani Asia.

Mipango ya silaha za nyuklia na makombora ya Korea Kaskazini inatarajiwa kuwa katika ajenda za mkutano huo. Pia viongozi hao watatu huenda wakabadilishana maoni juu ya masuala ya mateka.
###