Gavana wa Benki Kuu ya Japani ajadili yeni dhaifu na Waziri Mkuu Kishida

Gavana wa Benki Kuu ya Japani, BOJ Ueda Kazuo na Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio walijadili kuhusu kiwango cha ubadilishaji wa fedha za kigeni katika ofisi ya waziri mkuu jijini Tokyo jana Jumanne.
Mkutano huo unakuja huku yeni ikiendelea kushuka thamani kufikia viwango vya kuvunja rekodi dhidi ya dola.

Ueda aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kuwa yeye na Kishida walibadilishana mawazo kuhusu kushuka kwa kiwango cha ubadilishaji wa fedha.

Gavana wa BOJ alisema, kwa ujumla viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni vinaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi na bei.z

Pia alisema kuwa BOJ itafuatilia kwa karibu kushuka thamani kwa yeni hivi karibuni katika sera za usimamizi.

Mwezi uliopita, Ueda alisema “ndiyo” wakati mwandishi wa habari alipouliza ikiwa athari ya udhaifu wa yeni kwa bei kwa ujumla ilikuwa ndani ya viwango ambavyo vinaweza kupuuzwa.

Soko halikuona jibu lake kama ujumbe mzito wa kuendelea kufuatilia kushuka thamani kwa yeni, na sarafu hiyo ilidhoofika haraka baada ya hapo.

Alipoulizwa kuhusu hilo jana Jumanne, Ueda alisema hakuna mabadiliko katika msimamo huo, lakini benki kuu itaangalia kwa umakini jinsi udhaifu wa yeni utakavyoathiri kiwango cha msingi cha ongezeko la bei.
###