Putin aagiza mazoezi ya silaha za kimbinu za nyuklia

Maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi jana Jumatatu walisema kwamba Rais Vladimir Putin ameagiza maandalizi ya mazoezi ya maigizo ya kutumia silaha za kimbinu za nyuklia. Walisema wanataka kudumisha utayari wa vikosi vya mapambano na silaha zisizo za kimkakati za nyuklia.

Maafisa hao walisema kwamba mazoezi hayo ni jibizo kwa “matamshi ya kichokozi na vitisho vilivyotolewa na maafisa fulani wa nchi za Magharibi.” Walisema wanataka kuhakikisha uadilifu na uhuru wa eneo la Urusi.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov alisema kuwa baadhi ya viongozi wa nchi za Magharibi wamezungumzia “nia ya kutuma vikosi vya ziada vyenye silaha” nchini Ukraine. Aliongeza kuwa, “Hii ni awamu mpya kabisa katika kuongeza mzozo huo.”

Putin anaanza awamu ya tano mamlakani kama rais leo Jumanne. Alhamisi wiki hii, vikosi vyake vitaadhimisha kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kwa kusherehekea Siku ya Ushindi.
###