Putin asisitiza umuhimu wa usalama wa taifa wa Urusi katika hotuba yake ya kwanza

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesisitiza katika hotuba yake ya kwanza ya muhula mpya wa miaka sita kwamba ataweka maslahi na usalama wa watu wa Urusi mbele kabla ya kitu kingine.

Jana Jumanne, Putin aliapishwa katika muhula wake wa tano kama rais wa nchi hiyo.

Wakati mzozo kati ya Urusi na nchi za Magharibi juu ya uvamizi nchini Ukraine ukizidi, Putin alisisitiza kuwa usalama wa taifa na uthabiti vitakuwa vipaumbele vyake vikubwa zaidi.

Alisema kwamba Urusi ipo tayari kufanya majadiliano na mataifa ya Magharibi juu ya usalama na uthabiti wa kimkakati, lakini pande hizo zinapaswa kuwa sawa na kuheshimu maslahi ya kila upande.

Alisema, “Tumeungana na ni watu wenye nguvu, na kwa pamoja, tutaondokana na changamoto zote, kutimiza mipango yetu yote,
na pamoja tutashinda.”

Putin ambaye ana umri wa miaka 71, amekuwa maradakani kama rais ama waziri mkuu kwa miaka zaidi ya 20, tangu achukue madaraka ya urais kwa mara ya kwanza mwaka 2000.