Israel kutuma ujumbe nchini Misri wakati ikiendelea na operesheni mjini Rafah

Israel inasema itatuma ujumbe nchini Misri kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini pia operesheni zitaendelea mjini Rafah kusini mwa Gaza ili kuiwekea Hamas shinikizo la kijeshi.

Hamas ilitoa taarifa jana Jumatatu ikisema imewataarifu wapatanishi wa Qatar na Misri kwamba kundi hilo limekubali pendekezo lao la kusitisha mapigano.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilisema kwamba itatuma ujumbe nchini Misri “katika jitihada za kuongeza uwezekano wa kufikia makubaliano kwa masharti yanayokubalika kwa Israel.”

Lakini pia ilisema baraza la mawaziri la vita limekubaliana kwa kauli moja kuendelea na operesheni mjini Rafah ili kuiwekea Hamas shinikizo la kijeshi na kutoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na kundi hilo.

Runinga ya Al Jazeera inasema pendekezo la kusitisha mapigano lililokubaliwa na Hamas linajumuisha awamu tatu ambapo kila moja itadumu kwa siku 42.

Katika awamu ya kwanza, Hamas itawaachilia huru mateka 33, wakiwemo wanawake na watoto, kwa mabadilishano ya wafungwa wanaoshikiliwa na Israel.

Awamu ya pili inatoa wito kwa Israel kuondoka kikamilifu kutoka eneo la Gaza na Hamas kuwaachilia wanaume wote wa Israel wanaosalia, wakiwemo wanajeshi wanaoshikiliwa mateka.

Awamu ya tatu inajumuisha mpango wa ujenzi mpya kwa Gaza unaohusisha Umoja wa Mataifa na mataifa wapatanishi.

Inatimia miezi saba leo Jumanne tangu uvamizi uliosababisha vifo uliofanywa na Hamas nchini Israel na kuanza kwa mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza. ###