Biden azungumza na Netanyahu wakati Israel ikiwaambia watu waondoke baadhi ya maeneo ya mji wa Rafah

Msemaji wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Marekani John Kirby amesema Rais wa nchi hiyo Joe Biden jana Jumatatu alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Biden alimwambia Netanyahu kuwa Marekani haiungi mkono operesheni za ardhini mjini Rafah kusini mwa eneo la Gaza ambazo zitaweka maisha ya raia hatarini.

Jana Jumatatu, ofisi ya Netanyahu ilisema kuwa baraza lake la mawaziri la vita liliunga mkono kwa kauli moja kuendelea kwa operesheni ya kijeshi mjini Rafah ili kuongeza shinikizo kwa Hamas na kushinikiza kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa katika eneo la Gaza.

Hamas ilisema kwenye taarifa jana Jumatatu kuwa imekubali pendekezo la kusitisha mapigano.

Kirby aliashiria kuwa mazungumzo yamefikia hatua muhimu. Alisema: “Tunataka kuwaokoa mateka hawa, tunataka kusitisha mapigano kwa wiki sita, kuongeza msaada wa binadamu. Bado tunaamini kuwa kufikia makubaliano ni matokeo bora zaidi.”
###