Jengo laanguka Afrika Kusini na kuua watu wawili, makumi ya wengine wanaswa chini ya vifusi

Jengo la ghorofa nyingi linaloendelea kujengwa limeanguka nchini Afrika Kusini na kusababisha vifo vya watu wawili. Makumi ya wengine wamenaswa chini ya vifusi.

Tukio hilo limejiri kwenye jiji la George lililopo kusini magharibi mwa nchi hiyo muda mfupi baada ya saa nane mchana kwa saa za nchi hiyo. Wengi wa wafanyakazi wa ujenzi 75 waliathirika.

Mamalaka za nchi hiyo zinasema 22 kati ya wafanyakazi hao wameokolewa na kuhamishiwa hospitalini, lakini wawili walithibitishwa kufariki baadaye.

Kazi ya uokozi inaendelea kwa wafanyakazi wengine 53 waliosalia wanaoaminika kuwa wamenaswa chini ya vifusi.

Picha za video kutoka kwenye kamera za usalama zinaonyesha jengo hilo likianguka ghafla na wingu la vumbi jeupe likienea kote katika eneo hilo la makazi.

Maafisa wa jiji hilo na polisi wanapanga kuazisha uchunguzi juu ya chanzo cha jengo hilo kuanguka wakati wakiendelea na kazi ya uokozi.
###