Idadi ya vifo kufuatia mvua kubwa nchini Brazil yaongezeka hadi 83, watu zaidi 100 bado hawajulikani waliko

Mamlaka kusini mwa Brazil zinasema idadi ya vifo kutokana na mvua kubwa isiyopusa imeongezeka hadi 83 huku watu zaidi ya 100 wakiwa bado hawajulikani waliko.

Tangu mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, mvua iliyoweka rekodi ya zaidi ya milimita 500 imenyesha katika baadhi ya maeneo ya jimbo la kusini mwa nchi hiyo la Rio Grande do Sul.

Mvua hiyo kubwa imesababisha madhara kote jimboni humo, ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa, maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa sehemu ya bwawa.

Jana Jumatatu, maafisa wa eneo hilo walisema watu 83 wamethibiitishwa kufariki na wengine 111 bado hawajulikani waliko.

Janga hilo limelazimu watu zaidi ya 120,000 kuhama makazi yao na watu zaidi ya 870,000 wameathirika na kukatika kwa umeme na usambazaji wa maji na usumbufu mwingine.

Mamlaka za utabiri wa hali ya hewa nchini Brazil zinaonya kuwa mvua kubwa inaweza ikaanza tena kunyesha katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo kufikia Ijumaa wiki hii.
###