Marais Xi wa China na Macron wa Ufaransa wakutana, watoa wito wa kuepuka ‘Vita Baridi vipya’

Rais wa China Xi Jinping amemwambia mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kuwa nchi hizo mbili zinapaswa kufanya kazi pamoja kuepuka “Vita Baridi vipya.”

Xi alikutana na Macron mjini Paris jana Jumatatu. Hii ilikuwa sehemu ya ziara ya kwanza ya Xi barani Ulaya katika kipindi cha miaka mitano na ilifanyika wakati mmoja na maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Ufaransa.

Xi alimwambia Macron kuwa nchi zao zinapaswa kujaribu kudumisha uhuru na kuhamasisha mitazamo ya nchi nyingi zenye usawa na mpangilio duniani.

Katika mkutano wa pamoja na wanahabari baada ya mazungumzo kati yao, Macron alisema kuwa nchi hizo zitaweza kutekeleza wajibu muhimu katika kuhakikisha uthabiti wa dunia.

Viongozi hao pia walijadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Macron alisema Ufaransa inaunga mkono jaribio la China la kutoiuzia Urusi silaha zozote, na pia dhamira yake ya kuweka udhibiti mkali kwa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hiyo zinazoweza kutumiwa kwa ajili ya madhumuni ya kijeshi.

Xi alisema China imekuwa ikitekeleza wajibu katika juhudi za kuleta amani nchini Ukraine badala ya kuwa mtazamaji.

Viongozi hao pia walikubaliana kutoa wito wa usitishaji vita duniani wakati wa mashindano yajayo ya Olimpiki ya Msimu wa Joto mjini Paris.
###