Reuters: Mkuu wa CIA asafiri kuelekea Qatar huku kukiwa na mkwamo katika mazungumzo ya Israel na Hamas

Mkuu wa shirika la kijasusi la Marekani CIA, ameondoka kuelekea Qatar huku kukiwa na mkwamo katika mazungumzo ya Israel na Hamas kuhusu kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

Jana Jumapili, shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba Mkurugenzi wa CIA William Burns alikuwa akisafiri kwenda Doha kufanya mkutano wa dharura na waziri mkuu wa Qatar.

Wajumbe wa Hamas wameondoka Misri, bila makubaliano na Israel. Kundi hilo lilidai umalizaji kabisa wa mapigano.

Shirika la habari la Reuters lilimnukuu afisa mmoja akisema kuwa ziara ya Burns nchini Qatar "inalenga kutoa shinikizo kubwa kwa Israel na Hamas kuendelea kufanya mazungumzo."

Qatar na Misri zimekuwa zikisimamia mazungumzo hayo. Kiongozi mkuu wa mrengo wa kisiasa wa Hamas yuko nchini Qatar.

Vilevile jana Jumapili, wanajeshi wa Israel waliendelea kushambulia mji wa Rafah kusini mwa Gaza. Reuters inasema takribani watu 19 wameuawa.