Mazoezi ya gwaride la kijeshi kwa ajili ya Siku ya Ushindi yafanyika Moscow

Mazoezi ya gwaride la kijeshi kwa ajili ya Siku ya Ushindi itakayoadhimishwa Alhamisi yamefanyika mjini Moscow.

Siku ya Ushindi ni kumbukizi ya ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya Nazi ya Ujerumani katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Ni moja ya sikukuu muhimu zaidi nchini Urusi.

Gwaride la Siku ya Ushindi la mwaka huu litakuwa la tatu tangu Urusi kuivamia Ukraine. Vikosi vya Urusi kwa sasa vinazidisha mashambulizi yake mashariki mwa Ukraine.

Baadhi ya watu nchini Urusi wamesema nchi zingine ulimwenguni zinatambua kuwa mwisho wa siku Urusi itashinda vita hivyo. Wengine wamesema wanatumai ushindi wa Urusi na kurejea salama kwa wanajeshi wake, wakielezea faraja yao kwa mama na wake wa wanajeshi.

Lakini baadhi ya watu wamesema mapigano kati ya nchi hizo mbili si sawa na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na hawataona fahari yoyote bila kujali ikiwa Urusi itashinda au la.