Israeli, Serikali imeamua kufunga ofisi za Al Jazeera.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa serikali yake imeamua kufunga shughuli za kituo cha runinga cha satelaiti cha Al Jazeera nchini humo.

Netanyahu alitoa taarifa hiyo jana Jumapili kupitia mitandao ya kijamii, akielezea kuwa shirika hilo la habari lenye makao yake makuu nchini Qatar kama chaneli chochezi.

Al Jazeera ilitoa taarifa baadaye siku hiyo hiyo, ikishutumu uamuzi wa Israeli. Taarifa hiyo ilisema, “Mwendelezo wa Israel wa kukandamiza uhuru wa habari, unaonekana kuwa juhudi za kuficha vitendo vyake eneo la Gaza, ukiwa ni uvunjaji wa sheria za kimataifa na za kibinadamu.”

Bunge la Israel lilipitisha sheria mwezi uliopita inayoruhusu serikali kudhibiti vyombo vya habari vya kigeni inavyoviona ni hatari kwa usalama wa taifa.

Al Jazeera imekuwa ikiripoti kutokea Gaza kila siku tangu kuanza kwa mapigano ya hivi sasa ikiripoti madhara yaliyosababishwa na mashambulizi ya jeshi la Israel.

Ila Netanyahu amekuwa akishutumu namna chombo hicho cha habari kinavyoripoti. Wachambuzi wanadai kuwa sheria hiyo ilikuwa imelenga kuidhibiti Al Jazeera.