Xi awasili Paris, kufanya mazungumzo na Macron

Rais wa China Xi Jinping amewasili Paris nchini Ufaransa jana Jumapili, nchi ya kwanza katika ziara yake ya mataifa matatu barani Ulaya. Anatarajiwa kufanya mazungumzo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron leo Jumatatu.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Xi alitoa taarifa ya maandishi, akisema anatumai ziara hiyo itasaidia kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya China na Ufaransa na kufungua mustakabali mzuri wa uhusiano wa pande hizo mbili.

Ni safari ya kwanza ya Xi barani Ulaya katika kipindi cha miaka mitano. Pia atakwenda Serbia na Hungary hadi kufikia siku ya Ijumaa.

Xi na Macron wanatarajiwa kujadili uhusiano wa pande mbili wakati nchi hizo mbili mwaka huu zikiadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia.

Viongozi hao pia huenda wakabadilishana mawazo kuhusu hali ya Ukraine na Mashariki ya Kati, miongoni mwa masuala mengine.

Xi pia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya pande tatu nchini Ufaransa na Macron na Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen. Viongozi hao watatu watajadili uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya.

China inaonekana kujaribu kuimarisha uhusiano na Ufaransa, taifa kubwa la Ulaya lenye njia huru ya kidiplomasia, katika juhudi za kuiweka Marekani katika udhibiti.