Urusi yamweka Rais wa Ukraine Zelenskyy kwenye orodha ya wanaotafutwa

Wizara ya mambo ya ndani ya Urusi imesema imemweka Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kwenye orodha ya wanaotafutwa.

Juzi Jumamosi maafisa wa Urusi walitaja sababu ni ukiukaji dhidi ya kanuni za uhalifu za Urusi, lakini hawakutoa maelezo ya kina.

Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine ilijibu siku hiyo hiyo kwa kurejelea hati ya kukamatwa ambayo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Taarifa hiyo inasema ripoti kuhusu Zelenskyy kuwekwa kwenye orodha ya watu wanaotafutwa "zinadhihirisha jinsi serikali ya Urusi ilivyo tayari kufanya lolote na propaganda, ambapo wamekosa kitu kingine cha kubuni ili kuvutia nadhari."

Muhula wa tano wa Putin akiwa Rais wa Urusi utaanza kesho Jumanne. Nchi hiyo itaadhimisha kumbukumbu ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia siku ya Alhamisi wiki hii ambayo ni Siku ya Ushindi. Waangalizi wa mambo wanaona hatua hiyo ya Urusi kama jaribio jipya la kuhalalisha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kabla ya kuanza kwa muhula ujao wa Putin na maadhimisho ya kumbukumbu ya kumalizika kwa vita.