Japani yaahidi dola bilioni 1 kwenye mfuko wa ADB ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Japani imesema itachangia takriban yeni bilioni 160, au karibu dola bilioni 1.04 kwenye mfuko wa Benki ya Maendeleo ya Asia, ADB ili kusaidia nchi zenye kipato cha chini kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri wa Fedha Suzuki Shunichi amejadili juu ya mchango huo jana Jumapili katika mkutano wa kila mwaka wa ADB katika mji mkuu wa Georgia, Tbilisi.

Awali benki hiyo ilikubali kukusanya tena fedha ili kusaidia nchi wanachama zilizo maskini zaidi na zinazoendelea zilizo hatarini zaidi kwa dola bilioni 5.

Suzuki amesema nchi za Asia Pasifiki ni kiini cha kuchochea ukuaji wa uchumi duniani. Aliongezea kuwa kanda hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile umaskini na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia amesema kuwa Japani ipo tayari kutoa msaada kwa nchi za visiwa hivyo na maeneo mengine ambayo yapo hatarini na mabadiliko ya tabia nchi.